Posts

Showing posts from February, 2026

CHURA NAMBA 20! sehemu ya 1

Image
      1.Eneo la Kiwalani, Saa kumi za jioni, Meweka gari pembeni, Kumngoja abiria.   2.Kapungia kwa yakini, Na mimi sikumuhini, Karibu na kituoni, Breki nikakanyagia.   3.Akafika dirishani, Anitazama usoni, Na mtoto mgongoni, Ngata amemfungia.   4.Ndipo nikashuka chini, Nikazunguka pembeni, Nikaenda mlangoni, Ili kumfungulia.   5.”Chura namba ishirini, Karibu na Mkunguni, Ni mtaa wa mjini, Pesa ngapi tanambia?”   6.”Siyo pesa nyingi sini, Wewe ingia garini, Ninapaki Magomeni, Pale kama napitia!”   7.”Ningali nipo saluni, Siendi sasa nyumbani, Mpeleke Khalfani, Mwanangu anasinzia.”   8.”Chura namba ishirini, Muulize Yasmini, Mfanyakazi wa ndani, Au kwa kina Rukia.”   9.Akamuingiza ndani, Akamuweka kitini, Mwana yupo taabani, Na ndoto zinamjia.   10.”Kaka yangu samahani, Naomba uwe makini, Huyu afike nyumbani, Shika pesa mesikia?” ITAENDELEA